Powered by Blogger.

Friday 23 January 2015

UHUNI: Wakala ataka kumuuza De Gea Madrid kijanja

Posted by Unknown at 00:50 0 Comments


NI utoto wa mjini tu na kukomoana. Wakala wa kipa namba moja wa Manchester United, David de Gea, Jorge Mendes inadaiwa kuwa analazimisha dili la kumuuza kipa huyo mahiri kwenda Real Madrid ya Hispania.
Imedaiwa kuwa Mendes amekerwa na kitendo cha Manchester United kumbabaisha mteja wake mwingine, Radamel Falcao, ambaye hana maisha mazuri Old Trafford na anatumia hasira hizo kutaka kulazimisha kumuuza De Gea kwenda Santiago Bernabeu.
Mendes amelipeleka jina la De Gea katika meza ya mabosi wa Real Madrid kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kumhamisha mteja wake huyo, ambaye anahusudiwa na mabosi wa timu hiyo wanaomuona kama mbadala wa muda mrefu wa kipa wao wa sasa, Iker Casillas.
Na Madrid wako tayari kutoa dau la Pauni 50 milioni na kuvunja rekodi ya uhamisho kwa makipa ambayo mpaka sasa inashikiliwa na kipa wa Juventus, Gianluigi Buffon ambaye alihamishwa kwa dau la Euro 51 milioni kutoka Parma mwaka 2001.
Mendes anajulikana kwa kuwamiliki wachezaji wenye majina makubwa katika soka kwa sasa kama Falcao, De Gea, Angel Di Maria, Cristiano Ronaldo na wengineo. Uhusiano wake na Manchester United umekuwa imara tangu enzi za Sir Alex Ferguson ambaye amewahi kumuelezea Mendes kama ‘Wakala bora aliyekuwa akifanya naye kazi.”
Lakini uhusiano huo unaonekana kuvunjika baada ya kocha wa Man United, Louis van Gaal kumshambulia Mendes wiki iliyopita kwa maelezo yake aliyotoa kuhusu Falcao baada ya nyota huyo wa Colombia kupigwa benchi katika pambano dhidi ya Southampton.
Kwa sasa De Gea anachukuliwa kama mmoja kati ya makipa bora duniani na mkataba wake unatazamiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao. Man United inataka kumpa mkataba wenye thamani ya Pauni 200,000 kwa wiki lakini inadaiwa kuwa De Gea anavutika na uhamisho wa kurudi kwao Hispania.
De Gea ametwaa taji moja na Manchester United ambalo ni ubingwa wa Ligi Kuu England tangu alipohamia Old Trafford kutoka Atletico Madrid kwa dau la Pauni 17 milioni mwaka 2011.
Kama watamuuza De Gea Man United hawatapata pigo kubwa kwani wamefanikiwa kuinasa saini ya kipa wa zamani wa Barcelona, Victor Valdes ambaye aliwahi kucheza chini ya Van Gaal akiwa Barcelona 2002 mpaka 2003.

Tags:

Share This Post

Get Updates

Subscribe to our Mailing List. We'll never share your Email address.

0 comments:

ddsdfs


Powered by Blogger.
back to top