Nimesimama Kituo cha Daladala Mbezi Mwisho, saa moja asubuhi
kusubiri usafiri wa kuelekea kazini. Watu ni wengi, kila mmoja yuko
makini kufuatilia mabasi yanayoingia kituoni hapo.
Mara basi la Mbezi- Gongo la Mboto linawasili,
kabla hata halijasimama kushusha abiria, watu wanalikimbilia, wanajazana
mlangoni, wengine wanaingia ndani kupitia kwenye madirisha.
Mimi nisiye na nguvu, nimeamua kukaa pembeni, siwezi kuingia ndani ya basi katika staili ya kusukumana au kupitia dirishani.
Kutokana na tabu ya usafiri, nalazimika kusubiri
muda mrefu, huku pia nikitumia fursa hiyo kujifunza mengi kutoka kwa
abiria wenzangu tunaosubiri usafiri kituoni hapo.
Kuna jambo naliona, linanivutia. Naamua kuelekeza umakini wangu kwenye jambo hilo. Ni mavazi hasa waliyovaa wanaume.
Napoteza muda na kuhesabu ‘kimya kimya’, moja,
mbili, tatu, nne...nagundua wanaume wengi wamevaa suruali nyeusi. Katika
10, nabaini zaidi ya nusu rangi nyeusi ndiyo imetawala.
Kati ya idadi inayobaki, wamevaa suruali zenye
rangi mbalimbali. Najisemea moyoni…haiwezekani, narudia kuhesabu kwa
mara nyingine, majibu yaleyale.
Naendelea na utafiti wangu ofisini. Naangalia
mavazi waliovaa wenzangu, suruali nyeusi kila kona. Kati ya watano,
watatu suruali zao ni rangi nyeusi.
Kwa nini suruali nyeusi zimetawala?
Najiuliza, nataka kwenda mbali zaidi kujua sababu,
nafikia uamuzi wa kuwauliza baadhi ya wanaume na wanawake siri ya rangi
nyeusi.
Namuuliza George Ambindwile, mhadhiri Chuo Kikuu
Dar es Salaam, ambaye mbali na kumfahamu ni miongoni mwa watu wanaopenda
kuvaa suruali nyeusi.
Anasema wengi wanapenda suruali nyeusi kwa sababu,
kwanza hazina gharama kuzinunua, lakini pia rangi zake hazikeri kama
rangi nyingine.
Anaongeza: “Ni vigumu sana kumwona mwanaume amevaa suruali ya
rangi nyekundu, kijani au nyingine yenye rangi inayoweza kumfanya
kuonekana akiwa mbali.”
Ambindwile anasema kutokana na wanaume wengi
kufanya kazi za nguvu kama kwenye gereji, viwandani na kazi zingine,
suruali nyeusi huficha uchafu.
Kwa maelezo ya haraka haraka, alisema suruali nyeusi zinapendwa zaidi watu kwa sababu gharama yake ni nafuu.
Kwa upande wake, Zakaria Haule anasema yeye ni
mpenzi wa kuvaa suruali nyeusi na sababu kubwa anaitaja ni suala la
uchumi. “Suruali nyeusi hazina bei dukani, kwetu sisi walalahoi ndiyo
kimbilio letu,” anasema na kuongeza:
Kwa upande wake, Dennis Osward msimamizi wa kituo
cha kulea watoto yatima cha Mwanzo wa Nuru cha Victoria, anasema suruali
nyeusi ndivyo vazi sahihi la walalahoi.
Anasema: “Suruali nyeusi haifuliwi mara kwa mara
kwa sababu huficha uchafu tofauti na zingine. Kutofuliwa mara kwa mara,
kunaifanya kudumu muda mrefu.”
“Unahitaji usafi kidogo unapokuwa na suruali
nyeusi. Unaweza kuivaa zaidi ya mara tatu na kuendelea bila kuonekana
kama ni chafu.”
Jannifer Sumi naye hakuwa mbali na mjadala wa
suruali nyeusi. Anasema: “Wanaume wa kawaida siyo watu wa fasheni kama
wanawake, hivyo hupenda nguo rahisi kama suruali nyeusi.
“Fasheni huendana na rangi kadhaa, wanaume wengi
siyo wachaguaji wazuri wa rangi, lakini pia hawapendi rangi za
kuwaonyesha kirahisi mbele ya macho ya watu.”
Vazi pekee rahisi kwao ni rangi nyeusi. Sumi
anakubali kuwa kuna wanawake wengi pia hupenda rangi nyeusi, ingawa
sababu zinaweza kuwa tofauti na zile za wanaume.
Kwa upande wake, Noor Shija anasema wanaume hupendeza zaidi wanapovaa suruali za rangi nyeusi kuliko rangi nyingine yoyote.
Anasema: “Suruali nyeusi zina faida kubwa kuliko kinyume chake. Kwanza, ndiyo rangi unayoweza kuvaa na shati lenye rangi yoyote.
Pia, mtu anapovaa suruali nyeusi, anaweza kufunga mkanda wa rangi yoyote. Kwa ufupi, rangi nyeusi ndiyo inayowafaa wanaume.”
“Ukiwa na suruali nyeusi, unaweza kuvaa na shati lenye rangi yoyote, liwe shati la bluu, jekundu, jeupe na hata njano.
Sabato Mwakipesile, anayemiliki ofisi ya ushonaji
nguo ‘Pendeza Dress’ ya Mbezi Luis, anakiri wanaume wengi kupenda kuvaa
suruali nyeusi, akiwamo yeye mwenyewe.
Anasema katika ofisi yake, kati ya suruali 10
anazoshona kila wiki, sita huwa na rangi nyeusi na zinazobaki huwa na
rangi tofauti, lakini zinazokaribiana na nyeusi kama ‘Dark Blue’.
Anasema: “Mbali na kushona, pia nauza vitambaa
mbalimbali, lakini vile nyenye rangi nyeusi ndiyo vinapendwa zaidi na
wateja wanawake kwa wanaume.”
Kuhusu kwa nini wanaume wanapenda suruali nyeusi,
anasema: “Ni vazi rahisi, halichakai mapema, ni rahisi kuficha uchafu,
bei yake siyo kubwa na likishonwa vizuri linapendeza mwilini.”
Kwa upande wake, Jumanne Mussa mkazi wa
Kijitonyama, anasema wanaume wanapende suruali nyeusi kwa sababu ndiyo
tafsiri ya kupendeza kwa mwanaume.
Anasema: “Angalia viongozi au watu maarufu
duniani, vazi lao kubwa ni suti nyeusi. Hata kwenye sherehe za harusi,
bwana harusi hupendeza zaidi akiwa na suti nyeusi kuliko rangi
nyingine.”
Kwa upande wake, Lilian Timbuka anasema sababu
kubwa ya wanaume kupenda suruali nyeusi ni kwa sababu ya ‘upofu’ katika
kuchagua rangi.
“Wanaume siyo wachaguaji wazuri wa rangi, lakini
pia hawana mvuto na rangi kali au za kumeremeta. Macho yao ni mepesi
kuona rangi kali, lakini hawapendi rangi za aina hiyo,” anasema.
MAKALA KUTOKA GAZETI LA MWANANCHI.... Joseph Kapinga
MAKALA KUTOKA GAZETI LA MWANANCHI.... Joseph Kapinga
0 comments: